Uyoga unapangwa katika kundi la mimea kuvu, kundi ambalo ni tofauti sana na mimea ya kawaida (yenye rangi kijani), pia ni tofauti na wanyama na pia bakteria. Kuvu hukosa sifa kuu ya mimea ya kawaida kwa kutokuwa na uwezo wa kutumia nishati ya jua kwa kuwa kuvu haina rangi ya kijani.
Kwa hivyo basi kuvu hutegemea viumbe vingine kwa kufyonza uteute wa chakula toka viumbe hivyo inavyojishikiza kwake (au kuishi ndani yake). Maumbo ya kuvu yaliyo hai ni nyuzinyuzi ambazo huunda tandao wa nyuzinyuzi.
Katika hali muafaka ya mahali kuvu ilipo, kuvu kujibagua kijinsia na kijamii ili itoe mbegu vizalia. Hizo mbegu vizalia ndio uyoga.
Lile umbo linaloonekana, kimaumbile ndilo tunda na sehemu kubwa zaidi ya uyoga imo ndani ya mkatetaka au chini ya ardhi, hata katika gome la mti uliooza.
MAJINA YA UYOGA KISAYANSI NA KIBIASHARA
Katika kitabu hiki majina ya kisayansi yametumika, kwa vile hayaleti utata kulinganisha na lugha za kibiashara. Kwa mfano, uyoga unaoitwa “oyster”, una aina zaidi ya 20, kila aina ikiwa ina mahitaji tofauti ya joto muafaka, rangi tofauti na kima cha ukuaji ni tofauti.
Kwa wastawishaji wa uyoga, lililo muhimu zaidi katika suala la kutambua majina vizuri ni kutumia majina ya kisayansi. Ni vizuri zaidi kuagiza aina ya uyoga unayoihitaji kwa majina ya kisayansi unapowasiliana na wauzaji rasmi wa mbegu za uyoga.
MAZINGIRA YA KUVU (UYOGA)
Kuvu au uyoga hutegemea viumbe hai wengine kwa kujifyonzea chakula. Kuvu inaweza kupata chakula chake kwa hali aina tatu:
Ø Kufyonza mimea iliyoisha oza.
Ø Kuishi na mimea hai (hasa miti) kwa kutegemeana.
Ø Kuishi kama nyonyaji bila faida kwa mmea mwenza.
Hali hizi za kuishi hazina uhusiano na ulikaji wa aina yoyote ya uyoga. Uyoga unaolika na usiolika (wenye sumu) vyote huweza kutumia hali tatu zilizoainishwa. Hata hivyo, kitabu hiki kinazungumzia uyoga unaofyonza mimea iliyooza.
MASALIA YA MIMEA ILIYOOZA :
Kuvu zinazofyonza masalia ya mimea iliyooza budi ipate aina hii ya masalia. Katika hali ya kawaida katika maisha yake, kuvu huota katika majani yaliyooza, katika kinyesi cha wanyama kilichooza, na katika visiki vya miti iliyooza. Kuna aina nyingine za kuvu hupendelea kuota kwa kuozesha singa za ngozi za wanyama, wakati kuvu nyingine hupenda kuota kwa kuozesha manyoya ya ndege.
Kuvu zinazofyonza masalia ya mimea, huozesha viinilishe masalia na mimea au wanyama hai hunufaika na masalia ya mimea au wanyama yanapoozeshwa na kuvu ndani ya mkatetaka. Uyoga wa aina ya oyster huozesha jamii ya miti. Hivyo hustawishwa kutokana na masalia yoyote yenye seli za miti.
MZUNGUKO WA UHAI WA KUVU
Kuvu huzaliana kwa kutoa mamilioni ya mbegu za uyoga. Mbegu hizi zikitua mahali penye hali muafaka, ndipo huweza kuota na kutoa nyuzinyuzi. Hizo nyuzinyuzi zinapojibagua kijinsia na kujamiiana ndipo uyoga unaota.
UKOMAAJI WA MBEGU :
Katika utaratibu wa ustawishaji wa uyoga unaoliwa, zile mbegu huria zinazosambaa baada ya nyuzinyuzi kujibagua na kujamiiana, hizo hazitumiki. Ni kwa sababu mbegu hizo ni ndogo mno kushikika, pia ni kwa vile aina za uyoga haziwezi kuainishwa kikamilifu ili aina hii isichanganyikane na aina nyingine. Hata kuotesha mbegu huria za uyoga huchukua muda mrefu sana, ambavyo kuvu nyingine huoteshwa haraka zaidi. Hali inayoweza kutatiza wastawishaji uyoga.
Uyoga unaokufaa wewe budi usambae upesi ndani ya mkatetaka kabla ya kuvu zisizofaa au bakteria kujiotesha. Kufanikisha hali hii, nyuzinyuzi huoteshwa kabla, zikiwa safi bila vimelea vya kuvu zingine. Huoteshwa katika mkatetaka uliochemshwa sana kuua vimelea vinginevyo.
Nyuzinyuzi hizo ndio huitwa mbegu ya uyoga. Mbegu kama hii itaota haraka zaidi kabla ya kuvu zisizotakiwa, na kufanikisha ustawi wa uyoga halisi.
MUDA WA KUTUNZA MBEGU ( NYUZINYUZI)
Nyuzinyuzi za mbegu za uyoga husambaa ndani ya mkatetaka na kujifyonzea lishe iliyo ndani ya mkatetaka. Muda huu ndio huitwa muda wa kutunza. Baadaye lishe inapopungua katika mkatetaka, au hali ya joto inabadilika, nyuzinyuzi za mbegu ndipo zitafikia kipindi kiitwacho cha uzazi.
Hali ya joto ya nyuzijoto 25 celsius ni muafaka kwa hali hii ya mwisho wa muda wa kutunza (kuingia muda wa uzazi).
Aina nyingi za uyoga huafikiana na joto hili. Lakini hata hewa ya ukaa (CO ) inapoongezeka katika mazingira ya mbegu, nayo husababisha ukuaji haraka wa nyuzinyuzi za mbegu lakini hali hii haifai kwa kukomaa uyoga.
Mchoro Mzunguko wa uhai katika maisha ya uyoga
Mchoro Mzunguko wa maisha kuanzia na uyoga hadi mbegu kutokea.
Vyanzo vitokanavyo na minofu ya uyoga hutolewa katika uyoga na kupandwa katika mkatetaka unaofaa. Huu mkatetaka ukikomaa ndio hutumika kuzalisha uyoga.
Baada ya kusambaa nyuzinyuzi za mbegu za uyoga ndani ya mkatetaka, ndipo uyoga wenyewe hutokea. Uwingi na ubora wa uyoga huu vitatokana na mazingira.
Viashiria muhimu vya mazingira muafaka ni:
Ø Joto ibadilike.
Ø Unyevunyevu mwingi.
Ø Hewa iwe nyingi.
Ø Mwanga.
Viashiria hivi ni tofauti kati ya aina moja ya uyoga na nyinginezo. Viashiria vinavyosaidia kukomaa uyoga hudumaza hatua ya nyuzinyuzi za uyoga. Kwa hiyo budi mabadiliko ya viashiria yafanyike baada ya nyuzinyuzi kusambaa ndani ya mkatetaka. Kwa kweli hali inayodumaza ukuaji wa nyuzinyuzi, ndiyo inasaidia uyoga kuanza kukua.
Mifano miwili ya kusaidia kuonyesha ukuaji katika aina za uyoga:
? Baadhi ya aina za uyoga iitwayo oyster, kwa mfano Pleurotus ostreatus, hukua vema baada ya kufikia hatua ya kuwa nyuzinyuzi na pia kupatiwa mshituko wa kuteremshiwa joto kwa Celsius 5 hadi 10 ikiambatana pia na hewa ya ukaa kupunguzwa. Ukuaji katika hatua ya nyuzinyuzi unaweza kuendelea katika giza lakini ukomaaji huhitaji mwanga.
Aina ya uyoga iitwayo shiitake (Lentinula edodes) iliyokomaa yenye nyuzinyuzi zake katika mifuko ya mkatetaka ikilowekwa katika maji kwa muda wa siku moja au mbili hupata mshituko na kusababisha ukuaji wa uyoga. Mshituko huo huondoa hewa ya ukaa iliyo ndani ya mifuko.
Vichwa vidogo vya uyoga hujitokeza wakati inapoanza hatua ya uyoga kuzaliana. Katika hali inayofaa, hivi vichwa vidogo huwa uyoga. Lishe ya kukuza uyoga hutiririka kutoka katika nyuzinyuzi kwenda katika uyoga unaokua. Huo mtiririko husaidiwa na unyevunyevu wa maji yanapokuwa mvuke badala ya matone ya maji.
Ndiyo maana unapostawisha, uyoga huharibiwa na maji ya matone. Hali ya unyevunyevu iwe kimvuke.
JOTO MUAFAKA KATIKA UYOGA UNAOLIMWA
Chagua aina ya uyoga unaopendelea hali ya joto ya shambani mwako. Jambo hili litakuepusha kusumbuka na kugharimia marekebisho ya joto katika nyumba ya uyoga, pia kutakuondolea gharama kwa ajili ya nishati.
Aina inayoweza kustawi siku hizi katika nchi za joto la celsius 30 hivi, ni uyoga wa oyster (Pleurotus cystidiosus, Pleurotus abalones, Pleurotus ostreatus – var.florida) na aina ya Volvariela volvacea, agaricus bitorquis, stropharia rugoseannulata na aina iitwayo wood ear (Auricularia politricha) tu.
No comments:
Post a Comment